Matumaini ya timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Congo kufuzu kwa mara ya tatu mfululizo katika michuano ya soka
barani Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za nyumbani yameongezeka
baada ya kuifunga Cameroon bao 1 kwa 0 katika mchuano wa mzunguko wa
kwanza jijini Yaounde siku ya Jumatatu.
Leopards walipata bao lao la kipekee ugenini katika dakika ya
70 ya mchuano huo ulioahirishwa kwa saa 24 baada ya refarii kitoka
Sudan Khalid Abdel Rahman kuchelewa kuwasili kwa muda kuchezesha mchuano
huo.Cameroon walipata nafasi ya kusawazisha lakini kipa wa DRC Herve Lomboto aliuokoa mkwaju wa Ndzama Abouna baada ya kuzuia mashambulizi mengine kutoka kwa wachezaji wa Cameroon .
Mataifa hayo sasa yatakutana katika mchuano wa mwisho tarehe 31 mwezi huu wa nane jijini Kinsasha mchuano ambao Leopard wanahitaji sare kufuzu ilhali wapinzani wao kwa sababu walifungwa nyumbani watahitaji kufunga mabao 2 kwa 0 kujikatia tiketi.
Mchuano mwingine wa mwisho ambao pia unasubiriwa ni kati ya Angola na Msumbiji waliotoka sare ya kutofungana mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Maputo.
Washindi wa michuano hiyo miwili watajiunga na mataifa mengine kama Burkina Faso, Burundi, Congo, Ethiopia, Gabon, Ghana, Libya, Mali, Mauritania, Morocco, Nigeria, Uganda, Zimbabwe na Afrika Kusini.
Fainali hizo zitaanza kutifua vumbi kuanzia tarehe 11 mwezi Januari na kumalizika tarehe 1 mwezi Februari mwaka ujao.
Aucun commentaire:
Enregistrer un commentaire