mercredi 23 janvier 2013

Mali: Vikosi vya Ufaransa na vile vya Mali vinajiandaa kuelekea kaskazini zaidi mwa nchi hiyo

     
Wanajeshi wa Ufaransa wakilinda kwenye moja ya maeneo ya mji wa Diabaly ambao wameuchukua toka kwa waasi
Wanajeshi wa Ufaransa wakilinda kwenye moja ya maeneo ya mji wa Diabaly ambao wameuchukua toka kwa waasi
Reuters

Na Emmanuel Richard Makundi
Vikosi vya Serikali ya Mali kwa kushirikiana na wanajeshi wa Ufaransa wanatarajiwa kuanza operesheni mpya kuelekea kaskazini mwa nchi hiyo baada ya kutwaa mji wa Diabaly na Mopti.

Msemaji wa jeshi la Mali amesema kuwa kwa sasa vikosi vyao vinajitayarisha kuingia katika mji wa Gao na kisha Timbuktu miji ambayo kwa sehemu kubwa bado inashikiliwa na waasi wa Kiislamu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wizara ya mambo ya ndani imesema kuwa ndege za Ufaransa zilishambulia ngome muhimu za waasi hao jirani na mji wa Timbuktu kwenye makazi ambayo yanadaiwa kuwa ni ya aliyekuwa rais wa Libya marehemu Muamar Gaddafi.

Kufuatia mashambulizi hayo taarifa zinasema kuwa baadhi ya wapiganaji wa kiislamu waliuawa ingawa hakukuwa na idadi kamili iliyotolewa ya waasi ambao waliuawa.

Katika hatua nyingine Serikali ya Marekani hapo jana imetoa ndege zake kubwa za kijeshi kwaajili ya kuwabeba wanajeshi wa Ufaransa ambao wako kwenye operesheni nchini Mali.

Mbali na kutoa ndege hizo pia wamesaidia jeshi la Ufaransa kwa vifaa zaidi vya kijeshi kwa lengo la kuendelea kurahisisha operesheni inayofanywa na vikosi hivyo kuisaidia nchi ya Mali.
tags: Francois Hollande - Mali - Marekani - Ufaransa - Umoja wa Mataifa UN

Aucun commentaire:

Enregistrer un commentaire