dimanche 27 janvier 2013

Mali: ECOWAS kuongeza idadi ya wanajeshi wanaokabiliana na wapiganaji wa kiislamu eneo la kaskazini mwa Mali

Mkutano wa Viongozi wa ECOWAS
dw.de

Na Flora Martin Mwano
Mawaziri wa Ulinzi wa nchi za Magharibi mwa Afrika chini ya mwamvuli wa jumuiya ya kiuchumi ya nchi za magharibi mwa Afrika ECOWAS wameadhimia kuongeza idadi ya wanajeshi kutoka wanajeshi 4700 mpaka 5700 katika oparesheni ya kukabiliana na wapiganaji wa kiislamu kaskazini mwa Mali.

Maadhimio hayo yalifikiwa jana jumamosi katika mkutano wa viongozi hao uliofanyika mjini Abdijan kuangalia jitihada za uharakishwaji wa zoezi la upelekaji wa vikosi nchini Mali.

Wakati huo huo vikosi vya kijeshi vya Mali na Ufaransa vimefanikiwa kutwaa mji wa Gao uliokuwa chini ya wapiganaji wa kiislamu wanaoshikilia baadhi ya maeneo ya kaskazini mwa Mali tangu mapinduzi ya mwezi April mwaka jana.

Wizara ya ulinzi ya Ufaransa imesema oparesheni hiyo imefanikisha kuuteka uwanja wa ndege wa Gao na kuharibu vifaa vya waasi katika eneo hilo ambalo lilikuwa ngome ya waasi.

Kwa upande wake Marekani imeendelea kuunga mkono oparesheni hiyo na imeahidi kujaza mafuta ndege za kivita za Ufaransa zilizopo nchini Mali katika oparesheni ya kuwafurusha wapiganaji wa kiislamu wenye uhusiano na mtandao wa kigaidi duniani wa Al Qaeda.

Mjadala kuhusu Mali ni miongoni mwa ajenda kuu zitakazotawala mazungumzo ya Wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika AU ambao wanakutana jijini Addis Ababa Ethipia kujadili maswala mbalimbali yanayolikumba bara la Afrika.

Mambo mengine yanayopewa kipaumbele katika mkutano huo ni pamoja na hatma ya makubaliano kati ya Sudan na Sudan Kusini, mapigano ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na hali ya kisiasa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Aucun commentaire:

Enregistrer un commentaire