samedi 30 mars 2013

UN: Hali ya wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati ni mbaya

Wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, kwenye picha ya hivi karibuni wakimuunga mkono rais Bozize
Wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, kwenye picha ya hivi karibuni wakimuunga mkono rais Bozize
Reuters

Na Emmanuel Richard Makundi
Wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wameendelea kupitia katika kipindi kigumu baada ya kuangushwa kwa Serikali ya Rais Francois Bozize kutokana na kukosa huduma nyingi za kijamii ikiwemo matibabu na chakula.

Hospital nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati zimefurika wagonjwa kipindi hiki ambacho kumekuwa na uhaba mkubwa wa chakula katika Taifa hilo hali ambayo imeendele kuzua hofu kwa wananchi.
Serikali mpya inayoongozwa na kiongozi wa Muungano wa Seleka Michel Djotodia inaendelea kuhaha kurejesha hali kama ilivyokuwa awali huku Waziri Mkuu Nicolas Tiangaye akisema watawasaka majambazi wanaotumia jina lao.
Waasi wa Seleka wamelaumiwa na jumuiya ya Kimataifa kwa kusababisha hali ngumu kwa wananchi kutokana na uporaji uliofanywa na askari wake wakati wakiingia kwenye mji wa Bangui baada ya kuwazidi nguvu wanajeshi wa Afrika Kusini.
Kwa siku ya tano mfululizo wananchi kwenye miji mingi wanakosa huduma za maji na umeme kutokana na kuzimwa kwa mitambo inayotumika kuzalisha maji na nishati jambo ambalo linaendelea kuzusha hofu kuhusu hali ya usalama nchini humo.
Tayari rais Djotodia ametangaza kuwa anaunda Serikali mpya itakayokaa madarakani kwa muda wa miaka mitatu na kutengua katiba ya nchi hiyo kwa madai kuwa analenga kuleta utawala wa kidemokrasia hatua ambayo imekosolewa vikali.
Umoja wa Afrika AU tayari imeiondolea uanachama nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati huku Umoja wa Mataifa ukitarajiwa kuketi kuangalia namna ambavyo inaweza kuwaondoa waasi hao wa Seleka na kuleta utawala wa kiraia.

Aucun commentaire:

Enregistrer un commentaire