dimanche 10 mars 2013

Muungano wa CORD wateua Mawakili 10 katika kesi ya kupinga matokeo ya Urais wa Kenya

KENYA - 
Makala iliyochapishwa tarehe : Jumapili 10 machi 2013 - Taarifa za ivi karibuni : Jumapili 10 machi 2013
Rais mteule wa Kenya Uhuru Muigai Kenyatta ambaye ushindi wake unapingwa na muungano wa CORD
rfi

Na Flora Martin Mwano
Muungano wa kisiasa wa CORD wa nchini kenya ambao unaaongozwa na waziri mkuu anayemaliza muda wake Raila Odinga umewateua mawakili kumi kuwasilisha kesi katika mahakama ya juu kupinga kutangazwa kwa Uhuru Kenyatta kama Rais wa nne wa Taifa hilo.

Kikosi hicho cha mawakili kitaongozwa na wakili maarufu wa nchini Kenya George Oraro sambamba na Mawaziri Mutula Kilonzo, James Orengo na Ababu Namwamba. Wengine ni Mwanasheria Mkuu mstaafu Amos Wako, Gitobu Imanyara, Pheroze Nowrojee, Chacha Odera, Ambrose Rachier na Paul Mwangi.
Mawakili hao wanatarajiwa kuwasilisha kesi hiyo mahakama ya juu jumatatu hii na mahakama hiyo itakuwa na siku 14 kisheria kusikiliza na kuamua kesi hiyo.
Iwapo mahakama itabaini kuwa kulikuwa na dosari katika uchaguzi huo itatoa uamuzi wa Wakenya kurejea katika uchaguzi mwingine ndani ya siku sitini na iwapo hakutakuwa na dosari yoyote basi Rais mteule Uhuru Kenyatta na Naibu wake Wiliam Ruto wataapishwa mwezi Aprili mwaka huu.
Raila Odinga wa muungano wa CORD ambaye ni Waziri Mkuu anayemaliza muda wake alipata jumla ya asilimia 44 ya kura zote na kuangushwa na Uhuru Kenyatta wa muungano wa Jubilee aliyeibuka kinara baada ya kupata asilimia 50.07 ya kura zote.
Viongozi wa CORD wameendelea kuhimiza utulivu na kuwataka wafuasi wao kutojihusisha na uvunjifu wowote wa amani wakati wakitafuta haki mahakamani.
Raisi mteule Uhuru Kenyatta amewataka wananchi wa Kenya kuwa watulivu katika wakati huu na kuahidi kufanya kazi na wapinzani wake na pia kushirikiana na jumuiya za kimataifa.
tags: Kenya - Raila Odinga - Uhuru Kenyatta

Aucun commentaire:

Enregistrer un commentaire