mercredi 7 août 2013

Kenya: Chanzo cha moto uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta nchini Kenya bado kitendawili

Uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta ukiwaka moto
Uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta ukiwaka moto
cir.ca

Na Sabina Chrispine Nabigambo
Chanzo cha moto mkubwa uliozuka katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta nchini Kenya leo alfajiri na kusababisha ndege zilizokuwa zikitarajia kutua katika uwanja huo kuelekezwa katika viwanja vingine sambamba na safari kuahirishwa na uwanja kufungwa bado hakijabainika.

Kufikia majira ya saa tatu asubuhi moto huo mkubwa umeweza kudhibitiwa kutokana na jitihada zilizofanywa na zimamoto na wanajeshi nchini licha ya kukabiliwa na upungufu wa maji.

Msemaji wa ikulu Manoah Esipisu akizungumza na waandishi wa habari nje ya holi la   abiria wanaowasili, amesema kuwa kwa sasa jitihada zinafanywa ili kurejesha shughuli zote kama kawaida.

Wakati ndege za mizigo na zenye kufanya safari za ndani zinatarajiwa kuendelea baadaye hii leo, Esipisu amesema, hakuna muda ambao umetolewa kwa ajili ya safari za ndege za kimataifa kuanza upya.

Taarifa zinaeleza kuwa hadi sasa hakuna majeruhi wala maafa ambayo yamejitokeza ingawa moto ulikuwa mkubwa na kwamba vitengo vya abiria wanaowasili na uhamiaji vimeharibiwa kabisa.
Ndege kadhaa ambazo zilitarajiwa kutua uwanjani hapo kutoka Dubai na Hong Kong, zimeelekezwa kutua katika uwanja wa Port City uliko Mombasa na kwamba kwa sasa moto umedhibitiwa.
Uwanja huo umekuwa tegemeo kubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki, pamoja na ndege za kimataifa za masafa marefu zimekuwa zikitua katika uwanja huo kuunganisha safari kwenye kanda nzima.
Aidha barabara zote za karibu na uwanja huo zimefungwa isipikuwa kwa dharura na hakuna watu wanaoruhusiwa kukaribia uwanjani hapo .

Moto huo umezuka siku mbili baada ya safari kucheleweshwa kwa saa kadhaa baada ya upungufu wa mafuta ya ndege kutokea.

Aucun commentaire:

Enregistrer un commentaire