mardi 27 août 2013

DRC yajiongezea matumaini ya kucheza fainali za CHAN

Na Victor Melkizedeck Abuso
Matumaini ya timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kufuzu kwa mara ya tatu mfululizo katika michuano ya soka barani Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za nyumbani yameongezeka  baada ya kuifunga Cameroon bao 1 kwa 0 katika mchuano wa mzunguko wa kwanza jijini Yaounde siku ya Jumatatu.

Leopards walipata bao lao la kipekee ugenini katika dakika ya 70 ya mchuano huo ulioahirishwa kwa saa 24 baada ya refarii kitoka Sudan Khalid Abdel Rahman kuchelewa kuwasili kwa muda kuchezesha mchuano huo.

Cameroon walipata nafasi ya kusawazisha lakini kipa wa DRC Herve Lomboto aliuokoa mkwaju wa Ndzama Abouna baada ya kuzuia mashambulizi mengine kutoka kwa wachezaji wa Cameroon .
Mataifa hayo sasa yatakutana katika mchuano wa mwisho tarehe 31 mwezi huu wa nane jijini Kinsasha mchuano ambao Leopard wanahitaji sare kufuzu ilhali wapinzani wao kwa sababu walifungwa nyumbani watahitaji kufunga mabao 2 kwa 0 kujikatia tiketi.

Mchuano mwingine wa mwisho ambao pia unasubiriwa ni kati ya Angola na Msumbiji waliotoka sare ya kutofungana mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Maputo.

Washindi wa michuano hiyo miwili watajiunga na mataifa mengine kama Burkina Faso, Burundi, Congo, Ethiopia, Gabon, Ghana, Libya, Mali, Mauritania, Morocco, Nigeria, Uganda, Zimbabwe na Afrika Kusini.

Fainali hizo zitaanza kutifua vumbi  kuanzia tarehe 11 mwezi Januari na kumalizika tarehe 1 mwezi Februari mwaka ujao.

Aucun commentaire:

Enregistrer un commentaire