lundi 11 février 2013

Mahujaji 36 wauawa nchini India baada ya kumalizika kwa tamasha la kujisafisha dhambi


Baadhi ya mahujaji walioangamia

Na Victor Melkizedeck Abuso
Serikali ya India inasema mahujaji 36 wameuawa baada ya watu kukanyagana katika kituo cha reli wakati wa tamasha la dini ya Kihindi iliyohudhiriwa na zaidi ya watu Milioni 30 katika jimbo la Uttar Pradesh Kaskazini mwa nchi hiyo.

Mkasa huo ulitokea siku ya Jumapili wakati wa kumalizika kwa tamasha hilo la siku 55 ambalo huleta mkusanyiko mkubwa wa watu duniani.
Ripoti zinaeleza kuwa watu wengine 31 wamejeruhiwa katika mkasa huo wengi wao wakiwa watoto na wanawake ambao walikuwa wamemaliza tamasha la kuoga katika eneo la Kumbh Mela linaloaminiwa kuwa ukioga kwenye maji hayo, unasamehewa dhambi zako.

Serikali nchini humo imekanusha ripoti kuwa mkasa huo ulitokea baada ya daraja la wapita njia kuvunjika na kusababisha maafa hayo.
Waziri Mkuu Manmohan Singh amesema amesikitishwa mno na mkasa huo uliosababisha vifo vya mahujaji hao wa Kihindi pamoja na wale waliojeruhiwa.

Tamasha hilo hufanyika kila baada ya miaka 12 na kuwakutanisha zaidi ya watu Milioni 100 wanaojisafisha kwa siku 55 katika mito ya Yamuna,Sataswati na Ganges.
tags: India - Manmohan Singh

Aucun commentaire:

Enregistrer un commentaire