vendredi 26 juillet 2013

Mataifa jirani na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC yatakiwa kusitisha ufadhili wake kwa Kundi la Waasi la M23

JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA CONGO-UN - 
Makala iliyochapishwa tarehe : Ijumaa 26 julai 2013 - Taarifa za ivi karibuni : Ijumaa 26 julai 2013
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry akiwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban Ki Moon ambao wametaka mataifa jirani na DR Congo kuacha kufadhili Kundi la M23
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry akiwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban Ki Moon ambao wametaka mataifa jirani na DR Congo kuacha kufadhili Kundi la M23


Na Nurdin Selemani Ramadhani
Umoja wa Mataifa UN umetaka kumalizwa mara moja kwa ufadhili unaofanywa kwa Makundi ya Waasi ya nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC unaofanywa na mataifa jirani kitu kinachochangia kuendelea na vita Mashariki mwa Taifa hilo. Kauli hiyo imetolewa kwenye mkutano uliotishwa Jijini New York katika makao Makuu ya Umoja wa Mataifa UN ukiwa na dhamira ya kuangalia mbinu zinazofaa ili kumaliza machafuko yanayoendelea Mashariki mwa DRC kwa muda sasa. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry ambaye aliongoza mkutano huo amesema wakati umefika sasa kwa mataifa yanayofadhili Kundi la Waasi la M23 waache kufanya hivyo mara moja kitu kitakachosaidia kupatikana kwa amani.

Kerry aliuambia mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UNSC nchi yake imekuwa ikisitikishwa na taarifa za Kundi la Waasi la M23 kuendelea kupatiwa ufadhili kutoka kwa nchi jirani na DRC.

Waziri huyo wa mambo ya Nje ambaye alikuwa Rais wa Mkutano huo amesema wakati umefika kwa pande zinazolifadhili Kundi la Waasi la M23 kijeshi kuacha kufanya hivyo kwa kuwa wanaushahidi unaothibitsha madai hayo.
Mkutano huo wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UNSC uliwaleta pamoja wanachama kumi na tano wa kudumu pamoja na Rwanda lengo likiwa ni kuhakikisha mkakati madhubuti unakuwepo kumaliza vita vya Mashariki mwa DRC.

Uingereza, Ufaransa na Mataifa mengine wameungana na Kerry kutaka ufadhili wowote wa kijeshi kwa Kundi la Waasi la M23 usitishwe mara moja kwa ajili ya mustakabali mwema wa eneo la Ukanda wa Maziwa Makuu ICGLR.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban Ki Moon ametoa wito kwa pande zote yaani Serikali ya Kinshasa na Waasi wa M23 kurejea kwenye meza ya mazungumzo huko Kampala yanayosimamiwa na ICGLR.

Ban amekiri mazungumzo ni moja ya njia muafaka kabisa kumaliza mapigano yanyoendelea kushuhudiwa Mashariki mwa DRC kati ya jeshi la Serikali la FARDC na Kundi la Waasi la M23.

Naye Mjumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Ukanda wa Maziwa Makuu ICGLR Mary Robinson amekiri hatua ya kuendelea kufadhiliwa kwa Kundi la M23 inasikitisha na kuchochea machafuko zaidi.

Rwanda imekuwa ikinyooshewa kidole cha lawama kwa kuwasaidia Waasi wa M23 kupambana na Jeshi la FARDC na imesisitiza yenyewe inalengo la dhati kuhakikisha utulivu unakuwepo nchini DRC.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda Louise Mushikiwabo amesema utulivu wa taifa hilo unategemea zaidi hali ya usalama katika nchi jirani ya DRC hivyo wao wanaunga mkono juhudi zinazochukuliwa kumaliza vita hivyo.

Aucun commentaire:

Enregistrer un commentaire