samedi 8 décembre 2012

Utulivu warejea kwenye mji wa Goma baada ya kuwasili kwa wanajeshi wa Serikali

     
Wanajeshi wa FRDC wakishangiliwa na wananchi baada ya kurejea kwenye mji wa Goma
Wanajeshi wa FRDC wakishangiliwa na wananchi baada ya kurejea kwenye mji wa Goma
MONUSCO

Na Emmanuel Richard Makundi
Maelfu ya wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC, FRDC wamerejea kwenye mji wa Goma ikiwa ni majuma kadhaa toka wautelekeze mji huo kwa waasi wa M23 waliokuwa wanaushikilia kabla ya kuondoka.

Wanajeshi hao wamepokelewa kwa shangwe na wananchi wa mji wa Goma ambao awali miongoni mwao waligawanyika kuhusu vikosi vya Serikali na vile vya waasi wa M23 ambavyo viliuvamia mji huo.
Majeshi ya serikali ya Kongo yalilazimika kuondoka kwenye mji wa Goma baada ya Tangazo la serikali kuu kuwataka kufanya hivyo ili kunusuru umwagaji damu ambao ungeweza kutokea iwapo wangepambana na waasi wa M23.
Baadhi ya wananchi wameeleza kufurahishwa kwao na kurejea kwa wanajeshi hao, huku pia maofisa wa polisi wakianza tena kuchukua doria kwenye vituo vya polisi ambavyo walikuwa wamevitelekeza kwa waasi.
Kurejea kwa wanajeshi hao wa FRDC kulisimamiwa na vikosi vya Umoja wa Mataifa vya MONUSCO vilivyoko kwenye jimbo la Kivu ya Kaskazini na Kusini kwaajili ya kulinda usalama wa raia.
Mkuu mpya wa majeshi ya ardhini aliyeteuliwa hivi karibuni na rais Joseph Kabila, jenerali Gabriel Amisi ameapa kupambana na wapiganaji wa kundi la M23 ambao wametishia kurejea kwenye mji huo iwapo Serikali ya DRc haitafanya mazungumzo nao.
Wakati huohuo kumeripotiwa kuanza kurejea kwa hali ya usalama kwenye mji wa Goma huku shughuli mbalimbali zikiendelea kama kawaida.

Aucun commentaire:

Enregistrer un commentaire