jeudi 4 avril 2013

Serikali ya Afrika Kusini kuondoa wanajeshi wake Nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati baada ya vifo vya wanajeshi wake 13

Wanajeshi wa Jeshi la Afrika Kusini wakiwa kwenye doria za ulinzi wa amani Mjini Bangui nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati
Wanajeshi wa Jeshi la Afrika Kusini wakiwa kwenye doria za ulinzi wa amani Mjini Bangui nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati
Reuters/Luc Gnago

Na Nurdin Selemani Ramadhani
Serikali ya Afrika Kusini imetangaza mpango wa kuondoa wanajeshi wake waliopo nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa kazi ya kulinda amani baada ya wanajeshi wake kumi na watatu kupoteza maisha kwenye mapigano yaliyodumu kwa saa tisa. Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma ndiye ametangaza mpango wa kuondoa wanajeshi wao nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati kutokana na kuchukizwa na hatua ya kufanyika kwa uasi chini ya Muungano wa Seleka ulioangusha serikali ya Francois Bozize.

Zuma amesema uamuzi wa kuondoa wanajeshi wao nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati umechukuliwa baada ya kungushwa kwa serikali ya Bozize iliyokuwa na makubaliano na nchi hiyo ya kuwasaidia kulinda amani.
Kiongozi wa Afrika Kusini amesema operesheni yao nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati ilikuwa ni kutoa mafunzo kwa wanajeshi wa taifa hilo tangu kufanyika kwa mapinduzi lakini kwa sasa hawawezi kufanya hivyo tena.
Rais Zuma amekwenda mbali na kusema serikali yake haina uhusiano wowote na Utawala wa Muungano wa Upinzani unaongozwa na Michel Djotodia hivyo wanalazimika kuondoa wanajeshi wao huko Bangui.
Afrika Kusini iliombwa kupeleka wakufunzi wa kijeshi 26 kuwapa mafunzo wanajeshi wa Jamhuri ya Afrika ya kati kufuatia mapinduzi ya mwaka jana lakini baadaye waliongeza wanajeshi 200 zaidi.
Wanajeshi 13 wa Afrika Kusini walipoteza maisha na wengine 27 kujeruhiwa tarehe 23 mwezi Machi kufuatia Wapiganaji wa Muungano wa Seleka 3,000 kuvamia kambi yao na kuanza kushambulia na kutoka makabiliano ya silaha yaliyodumu kwa saa tisa.
Serikali ya Afrika Kusini imekuwa ikikosolewa kwa hatua yake ya kupeleka wanajeshi nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati huku baadhi ya watu wakisema mpango huo ni sehemu ya biashara baina ya nchi hizo mbili.
Waziri wa Ulinzi Nosiviwe Mapisa-Nqakula amejitokeza na kukanusha madai na tuhuma hizo na kusema wanajeshi wao walienda nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati ikiwa ni sehemu ya mpango wa kulinda amani tu.

Aucun commentaire:

Enregistrer un commentaire