mardi 29 octobre 2013

Raia wa Norway ashukiwa ugaidi Kenya

 18 Oktoba, 2013 - Saa 06:49 GMT
Mabaki ya gari katika shambulio la Westgate

Polisi nchini Norway wanamchunguza Hassan Abdi Dhuhulow, kuhusu shambulio la kigaidi katika kituo cha biashara cha Westgate nchini Kenya karibu mwezi mmoja uliopita.
Mtuhumiwa huyo mwenye umri wa miaka 23, raia wa Norway mwenye asili ya Somalia, anashukiwa kusaidia mpango wa kufanyika kwa shambulio hilo.
BBC imezungumza na mmoja wa ndugu wa mtuhumiwa aliyeko nchini Norway, ambaye amesema, Hassan Abdi Dhuhulow aliondoka kutoka mji wa Larvik kwenda Somalia mwaka 2009.
Watu wapatao 67 waliuawa katika shambulio hilo mjini Nairobi, ambapo kundi la al-Shabaab lenye uhusiano na kundi la kigaidi la al-Qaeda lilikiri kuhusika na shambulio hilo.

Wiki iliyopita shirika la ujasusi la Norway, PST, lilisema kuwa limewatuma maafisa wake nchini Kenya kuthibitisha taarifa hizo kwamba raia wa Norway alihusika katika shambulio la Westgate, lililoanza tarehe 21 Septemba na kudumu kwa siku nne.
Bado haijafahamika ni wapiganaji wangapi walihusika. Awali polisi wa Kenya walikadiria kuwepo kwa washambuliaji kati ya 10-15 katika kituo cha kibiashara cha Westgate, lakini picha za CCTV ambazo zimekwishatolewa na serikali ya Kenya, imewaonyesha washambuliaji wanne.

Hassan Abdi Dhuhulow anaaminika kuwa mmoja kati ya watu wanne walionekana katika picha za CCTV.
Wachunguzi wa vinasaba bado wanaendelea na kazi ya uchambuzi wa mabaki na vifusi katika eneo la Westgate na hakuna miili zaidi iliyogundulika na haifahamiki kama washambuliaji hao waliuawa au bado ni hai.

Aucun commentaire:

Enregistrer un commentaire