jeudi 31 octobre 2013

Jeshi la DRC ladhibiti ngome ya mwisho ya M 23 ya Bunagana

Jeshi la DRC katika mji wa Bunagana

Na Victor Melkizedeck Abuso
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo limefanikiwa kuchukua udhibiti wa ngome ya mwisho ya waasi wa M 23 mjini Bunagana Mashariki mwa nchi hiyo karibu na mpaka wa Uganda.

Msemaji wa serikali ya DRC Lambert Mende ameliambia Shirika la Habari la Ufaransa AFP kuwa mafanikio ya jeshi la serikali sasa yanatoa nafasi ya kuendelea kwa mazungumzo ya amani kati ya kundi hilo na wajumbe wa serikali.
Ripoti zinasema kuwa, waasi wa M 23 waliokuwa wanapiga kambi katika ngome yao ya kijeshi ya Bunagana wanaelezwa kutorokea kusikojulikana huku kiongozi wa kundi hilo Betrand Bissimwa akiripotiwa kukimbilia nchini Uganda.
Serikali ya Uganda imethibitisha kuwa Bissimwa yuko nchini humo baada ya kuitwa na msuluhishi Mkuu wa mazungumzo ya amani kati yao na serikali ya DRC Crispus Kiyonga.
Mwakilishi wa serikali ya Kinsasha katika mazungumzo hayo ya amani Francois Muamba, amedokeza kuwa ikiwa kundi la M 23 litakubali mapendekezo waliyotoa basi kuna matumaini kuwa suluhu likapatikana haraka.
Rais Joseph Kabila amesema kuwa bado kuna nafasi ya upatikanaji wa suluhu kupitia mazungumzo ya kisiasa na diplomasia na waasi hao na hivyo wanastahili kuweka silaha chini au wataendelea kushambuliwa kijeshi.
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa MONUSCO katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Martin Kobler mapema juma hili aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa kundi la waasi la M 23 sio tishio tena kijeshi Mashariki mwa nchi hiyo.
Kobler alieleza kuwa waasi wa M 23 wametoroka katika kambi zao za kijeshi na sasa wanajificha karibu na mpaka wa Rwanda baada ya kulemewa na wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wakisaidiwa na wale wa Umoja wa Mataifa.
Mapigano kati ya waasi na majeshi ya serikali yalianza wiki iliyopita baada ya mazungumzo ya amani kuvunjika jijini Kampala Uganda na kufikia siku ya Jumatatu jeshi la serikali lilifanikiwa kuchukua miji ya Rutshuru, Kiwanja na Rumangambo yote ambayo hapo awali ilikuwa inathibitiwa na waasi hao kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Kurudishwa nyumba kwa waasi hao kwa mujibu wa mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini DRC ni ishara tosha waasi hao wamedhoofishwa kijeshi na huenda huu ndio ukawa mwisho wao.
Hata hivyo, waasi hao wa M 23 wanasema kuwa wamejiondoa katika ngome zao kwa muda tu ili kuuonesha ulimwengu kuwa wao hawataki vita kwa mujibu wa rais wa kundi hilo Betrand Bissimwa.

Aucun commentaire:

Enregistrer un commentaire