samedi 30 mars 2013

Madaktari: Afya ya mzee Mandela yaendelea kuimarika

Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Mzee Nelson Mandela
Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Mzee Nelson Mandela
Reuters

Na Emmanuel Richard Makundi
Hali ya Afya ya Rais wa kwanza Mzalendo nchini Afrika Kusini Nelson Mandela maarufu kama Madiba imeanza kutengamaa ikiwa ni saa zaidi ya ishirini na nne tangu afikishwe Hospitali kwa matibabu ya maradhi ya mapafu yanayomsumbua.

Daktari ambaye anamhudumia Madiba amesema hali yake imeanza kuimarika na kama ataendelea hivyo basi muda si mrefu anaweza akaruhusiwa kurejea nyumbani baada ya matibabu.
Mandela mwenye umri wa miaka tisini na nne kwa sasa anaendelea kupatiwa matibabu ambapo kutetereka kwa afya yake kumewagusa wananchi wengie wa Afrika Kusini ambao wameendelea kutuma salamu za pole kwa kiongozi huyo.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu ya rais Jackob Zuma imesema kuwa, anamtakia heri mzee Madiba apone haraka na kusisitiza wananchi wa kumuombea kwa Mungu ili amponye na kurejea kwenye hali yake ya kawaida.
Mbali na rais Zuma kumtakia heri kiongozi huyo, pia rais wa Marekani, Barack Obama ametuma salamu za wananchi wa Marekani kumtakia heri mzee Madiba ambaye amemueleza ni kiongozi aliyekuwa mwanamapinduzi na mpenda maendeleo ya bara la Afrika.
Hii ni mara ya nne kwa Rais huyo wa zamani wa Afrika Kusini anayetambulika kama Baba wa Taifa Nelson Mandela kufikishwa Hospital kwa matibabu kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya mapafu.

Aucun commentaire:

Enregistrer un commentaire