mardi 12 novembre 2013

Uganda: Mazungumzo ya Kampala kuendelea licha ya kukwama kwa shughuli ya utiwaji saini kati ya DRC na waasi wa M23

DRC-M23-UGANDA - 
Makala iliyochapishwa tarehe : Jumanne 12 novemba 2013 - Taarifa za ivi karibuni : Jumanne 12 novemba 2013

Waziri wa mambo ya nje wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, Raymond Tshibanda
Waziri wa mambo ya nje wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, Raymond Tshibanda
Reuters

Na Emmanuel Richard Makundi
Siku moja baada ya kushindikana kutiwa saini kwa mkataba wa amani kati ya Serikali ya Kinshasa na waasi wa M23, utawala mjini Kampala unasema mazungumzo ya amani yataendelea licha ya kukwama kwa shughuli hiyo.

Serikali ya Uganda kupitia kwa msemaji wake, Ofwono Opondo, amethibitisha kuwa nchi hiyo inafanya juhudi za kuwakutanisha tena kwenye meza moja wajumbe wa Serikali ya DR Congo na wale wa waasi kujaribu kufikia muafaka kwenye masuala tata.
Hapo jana ujumbe wa Serikali ya Kinshasa ulishindwa kutokea kwenye eneo la tukio ambako kungefanyika shughuli ya utiaji saini mkataba wa amani kwa kile ilichoelezwa kuwa ujumbe huo haukuridhishwa na baadhi ya masuala ambayo yalikuwemo kwenye mkataba huo.
Kwenye mahojiano maalumu na mwandishi wa rfikiswahili, waziri wa mambo ya kigeni wa DR Congo, Raymond Tshibanda amethibitisha ujumbe wa nchi yake kutoshiriki zoezi la utiaji saini kwasababu mbalimbali ikiwemo kutoridhishwa na baadhi ya vifungu vilivyokuwemo kwenye mkataba huo.
Ujumbe wa Serikali ya Kinshasa unasema kuwa haukuridhishwa na baadhi ya vifungu ambavyo vimejumuishwa kwenye mkataba huo na pia suala la wao kutiliana saini na waasi halipo kwasababu walishawamaliza mashariki mwa nchi hiyo.
Licha ya ugumu wa kufikia makubaliano, serikali ya Uganda inasema kuwa mazungumzo yao bado hayajakwama na kwamba wanaendelea na juhudi ya kuzikutanisha pande hizo mbili kujaribu kumaliza tofauti zao.
Kando ya mkutano huo kumeibuka taarifa kuwa ujumbe wa DR Congo unataka kwanza nchi ya Rwanda ifanye mazungumzo na waasi wa FDLR na pia Serikali ya Uganda ifanye mazungumzo na waasi wa ADF-Nalu wanaopigana mashariki mwa nchi hiyo.
Kumezuka hofu ya kutokea tena machafuko mashariki mwa nchi hiyo iwapo makundi haya mawili hayatamaliza tofauti zao na Serikali za Rwanda na Uganda.
tags: Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo - Kundi la Waasi la M23 - Ofwono Opondo - Raymond Tshibanda - Rwanda - Uganda

Aucun commentaire:

Enregistrer un commentaire