mardi 12 novembre 2013

Ujumbe wa Serikali ya DRC wasusia shughuli ya utiaji saini mkataba wa amani na kundi la M23

DRC-M23-UGANDA - 
Makala iliyochapishwa tarehe : Jumanne 12 novemba 2013 - Taarifa za ivi karibuni : Jumanne 12 novemba 2013

Baadhi ya wajumbe wa mazungumzo ya Kampala wakiwa kwenye ukumbi wa mkutano huku ujumbe wa DRC ukiwa haupo
Baadhi ya wajumbe wa mazungumzo ya Kampala wakiwa kwenye ukumbi wa mkutano huku ujumbe wa DRC ukiwa haupo
Reuters

Na Emmanuel Richard Makundi
Ujumbe wa Aerikali ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo DRC na ule wa waasi wa M23 wameshindwa kutiliana saini mkataba wa amani kumaliza machafuko mashariki mwa nchi hiyo, katika tukio ambalo limeelezwa linalemaza juhudi za kupata amani kwenye eneo hilo.

Sherehe za utiwaji saini zilitarajiwa kufanyika mjini Kampala Uganda ambapo ujumbe wa Serikali ya DRC, ujumbe wa waasi wa M23 ukiongozwa na Betrand Bisimwa, ujumbe wa serikali ya Uganda na ule wa Umoja wa Mataifa wote kwa pamoja walifika kwa wakati kwenye eneo la tukio lakini wakashindwa kutia saini.
Msemaji wa Serikali ya Uganda, Ofwono Opondo amethibitisha kutofanyika kwa shughuli za utiwaji saini makataba wa amani kati ya kundi hilo na ujumbe wa Serikali ya DRC kwa kile alichoeleza kuwa ni kushindwa kufika kwa wakati kwa ujumbe wa DRC.
Opondo ameongeza wakati ujumbe wa M23 ukiongozwa na Bisimwa ukiwa umefika kwenye eneo la tukio, kwasababu zisizojulikana ujumbe wa Serikali ya DRC haukuweza kufika wala kutoa sababu za kwanini wameshindwa kutia saini mkataba huo.
Kushindwa kutiwa saini kwa mkataba wa amani baina ya pande hizo mbili kumeonekana kama pigo kwa juhudi za jumuiya ya kimataifa ambayo mara zote imetaka kuona suluhu inapatikana mashariki mwa nchi hiyo.
Hata hivyo shughuli za utiwaji saini zilikosolewa kwa sehemu kubwa na wachambuzi wa mambo ambao walikuwa wanahoji uhalali wa kusainiwa kwa mkataba huo wakati huu ambapo waasi wa M23 hawafanyi tena shughuli zao mashariki mwa nchi hiyo baada ya kufurushwa na majeshi ya Serikali FARDC.
Akizungumza baada ya kushindikana kwa mazungumzo haya, waziri wa mambo ya nchi za nje wa DRCongo, Raymond Tshibanda amesema licha ya ushindwa kufikia muafaka kwasasa, Serikali ya Kinshasa bado inania ya kuleta amani ya kudumu mashariki mwa nchi hiyo.
Tshibanda ameongeza kuwa, Serikali yake imekuwa ikishiriki mazungumzo ya amani mjini Kampala kwa miezi kadhaa hivi sasa na mara zote wamekuwa wakikutana na vikwazo na mambo ambayo ni ya muhimu kwa upande wao kufikia makubaliano kabla ya kutia saini.
Balozi wa Umoja wa Mataifa kwa nchi za maziwa makuu Mary Robinson ameeleza kusikitishwa kwake na kushindwa kutiwa saini kwa mkataba wa amani, na kuongeza kuwa iwapo zoezi hilo lingefanyika ingekuwa ni hatua muhimu sana kwa pande hizo mbili na kwa mustakabali wa eneo zima la maziwa makuu.
katika hatua nyingine, Serikali ya Uganda imesisitiza kuwa haitawakabidhi viongozi wa kijeshi wa kundi la M23 kwa Serikali ya DRCongo mpaka pale nchi hiyo itakapotia saini mkataba wa amani na pia kupata ruhusa toka kwa Umoja wa Afrika AU na nchi za Maziwa Makuu.
tags: Bertrand Bisimwa - Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo - Kundi la Waasi la M23 - Mary Robinson - Ofwono Opondo - Raymond Tshibanda - Uganda - Umoja wa Mataifa UN

Aucun commentaire:

Enregistrer un commentaire