Upinzani DRC wakubali kushiriki mazungumzo kwa masharti
Etienne Tshisekedi wakati wa kikao cha ufunguzi cha mkutano wa viongozi wa upinzani wa DRC, Juni 8, 2016 Genval, Ubelgiji.
THIERRY CHARLIER / AFP
Kiongozi mkuu wa upinzani
nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Etienne Tshisekedi, amesema
yuko tayari kwa mazungumzo na rais Joseph Kabila lakini ametoa sharti
kuwa mazungumzo hayo yafanyike chini ya usimamizi wa jumuiya ya
kimataifa.
Akizungumza mara baada ya
kuhitimisha mkutano wake na wanasiasa wengine wa upinzani aliowaalika
mjii Brussels, Ubelgiji, Tshisekedi, amesema walikutana kama wazalendo
kwa lengo la kubadilishana mawazo kuhusu namna ya kuhakikisha rais
Kabila hawanii urais kwa muhula wa tatu.Viongozi hao wamekubaliana kufuata njia za kisheria na amani kuhakikisha Rais Kabila anaondoka madarakani, na wao kujiepusha na vurugu ambazo huenda zikaifanya Serikali kutumia nguvu kuwakabili.
Katibu mkuu wa chama cha upinzani cha MSR, Nzangi Butondo, ameridhishwa na mkutano huo akisema ni wakihistoria, kwani ni kwa mara ya kwanza upinzani kukutana kwa kuweka wazi utaratibu wa kumaliza tofauti zao na kutazama njia ya kupambvana kisiasa nchni humo.
Mkutano huu umefanyika wakati ambapo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya nje wa Ubelgiji, Didier Raynders akiwa ziarani katika nchi za Maziwa Makuu kujaribu kushawishi kusaidia kupata suluhu ya mzozo wa kisiasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.